Ufugaji wa kuku una faida kubwa, lakini mkulima anatakiwa kuzuia kadri awezavyo uwezekano wa kuwepo magonjwa shambulizi.
Wafugaji wengi wamekuwa wakiwekeza katika ufugaji wa kuku. Ufugaji huo unalenga kuku wa kisasa au wa kienyeji. Wanajenga mabanda, kununua chakula, pamoja na kuku, wakitarajia kupata faida kubwa kutokana na uwekezaji huo. Hata hivyo, mradi unapoanza mambo huonekana kwenda sawa, mpaka mfugaji anaposhtuliwa na mlipuko wa magonjwa ambayo hupunguza uzalishaji au kuua kuku.
Mfugaji anaweza kufanya nini kupunguza hatari hii?
Mbinu zinazotumiwa na wakulima duniani kote zinanaonesha kuwa kuweka banda katika hali ya usafi, kuwalisha kuku ipasavyo na kuwapatia maji safi, ndiyo njia ya kwanza muhimu ya kupambana na magonjwa, kama vile mharo mwekundu, kipindupindu cha kuku, na ndui. Kuwa makini katika ufugaji wa kuku ni pamoja na kutoa chanjo kwa kuku, kuzuia magonjwa kama sotoka au ndigana na ndui.
Taratibu za kufuata ili kuzuia magonjwa
Utunzaji wa banda la kuku
• Ni lazima nyumba ya kuku iwe safi na kavu muda wote
• Nyumba ya kuku iwe na nafasi za kupitisha hewa ya kutosha ili kuepuka joto na unyevunyevu
• Hakikisha unaondoa matandazo na takataka zote kwenye banda wakati wote. Matandazo na taka zinaweza kuwa mbolea nzuri ya mboji kwa mimea yako.
• Fagia banda na kuhakikisha ni safi wakati wote. Weka matandazo mapya mara kwa mara.
• Weka nafasi ya kutosha kuku kupumzikia, viota vya kutosha, na kuweka maji sehemu ambayo ni rahisi kusafisha.
• Hakikisha unaondoa wanyama kama panya na wadudu nyemelezi kwenye sehemu ya malisho ya kuku kwani wao hubeba vimelea vya magonjwa.
Utunzaji wa kuku
• Toa chanjo muhimu kwa kuku ili kuzuia magonjwa kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa mifugo. Chanjo huanza katika wiki ya kwanza (mfano chanjo ya kuzuia sotoka) na inaweza kurudiwa baadaye.
• Epuka kuweka kuku wengi mahali pamoja kwani ni rahisi magonjwa kuenea kwa haraka kuku wanaporundikana.
• Tenganisha vifaranga na kuku wakubwa (isipokuwa kutoka kwa mama) kwa sababu vifaranga ni rahisi na wepesi sana kushambuliwa na magonjwa.
• Weka mipaka na madaraja ya sehemu za kuku kuzunguka/kucheza.
Ulishaji
• Wapatie kuku chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote. Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini, au maganda ya mayai.
• Wapatie kuku maji safi muda wote. Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.
• Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea kila siku. Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.
• Nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi.
• Hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi.
• Usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo. Kukabiliana na magonjwa
• Muone mtaalamu wa mifugo mara uonapo dalili zozote za kuumwa kwa mifugo wako.
• Watenge na uwapatie tiba au kuwaua na kuteketeza kabisa kuku wagonjwa kuepuka kuenea kwa magonjwa.
• Ondoa ndege waliokufa mara moja, uwafukie au kuchoma moto. Usile kuku aliyekufa. Baadhi ya magonjwa ya ndege yanaweza kuambukizwa kwa binadamu.
• Endapo kuna mlipuko wa ugonjwa katika eneo lako, usiruhusu watu kutembelea banda lako. Watu wanaweza kuleta maambukizi kwa miguu yao katika mabuti, nguo na mikono. Pia magari yanaweza kuleta madhara kwa mabanda yako kupitia matairi na upakuaji wa mizigo.
Ukaguzi wa mara kwa mara
Kila siku
• Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea pamoja na viota.
• Ondoa kinyesi.
• Waangalie kuku wako kwa makini ili kujua afya na maendeleo yao.
Kwa wiki
• Ondoa matandazo machafu na kuweka mapya.
Kwa mwezi
• Angalia uwepo wa wadudu na chawa, kisha utibu kama kuna ulazima.
Zingatia haya kabla ya kuleta mifugo wapya bandani
1. Ondoa matandazo yote, vyombo vya kulishia na kunyweshea.
2. Ondoa uchafu wote unaoonekana bandani.
3. Safisha banda lote kwa kutumia maji na dawa.
4. Suuza na uache likauke.
5. Puliza dawa ya kuua wadudu.
6. Weka matandazo mapya, weka viombo vya kulishia na kunyweshea.
No comments:
Post a Comment