MAELEZO YA MSINGI KUHUSU KILIMO CHA MBOGA MBOGA-Vegetables
Mboga
ni mmea au sehemu yoyote ya mmea inayoweza kuliwa na binadamu ambayo haina
sukari kama matunda. Mboga huweza kuliwa zikiwa zimepikwa na mara nyingi
huwekewa chumvi ili kuongeza ladha na pia huweza kuliwa zikiwa mbichi kwa mfano
kwenye kachumbari. Mboga ni sehemu muhimu sana katika mlo uliokamilika, hii
imesababisha ukuaji wa kasi wa soko la mboga na upandaji wa mboga katika maeneo
mengi ya mijini na vijijini.
Sehemu za mmea ambazo zinaweza kutumika kama mboga
I. Majani
Mboga
nyingi hutoka kwenye majani ya mimea. Mara nyingi haya majani huwa ya rangi ya
kijani kwasababu ya kutengeneza chakula cha mmea kutoka kwenye mionzi ya jua na
huwa na virutubisho vingi muhimu katika mwili wa binadamu kwa vile vitamin.
Miongoni mwa majani ambayo huliwa kama mboga ni Kabichi, Spinach, Chinese,
Mchicha na figiri.
II. Mizizi
Mizizi
ya baadhi ya mimea ni mboga nzuri na ina virutubisho kama vile vitamin A ambayo
huimarisha macho na kuongeza uwezo wa kuona. Miongoni mwa mizizi ambayo huliwa
kama mboga ni karoti.
III. Tunda
Tunda
kwa maana ya kibustani ni sehemu ya mmea ambayo hubeba mbegu na inalika ikiwa
mbichi au imepikwa. Mfano wa mimea ambayo sehemu ya tunda ni mboga ni kama vile
nyanya, matango, bilinganya na bamia.
IV. Bulb (Tunguu)
Hii
ni sehemu ya mmea ambayo hukua chini ya ardhi kwa mfano vitunguu (maji na
swaumu). Mboga za aina hii ni muhimu sana katika mwili wa binadamu kwani
husaidia kusafisha damu na huongeza ladha na harufu nzuri katika chakula.
V. Tuber (Kiazi)
Hii
ni aina ya mboga ambayo ni mzizi unaohifadhi chakula cha mmea. Aina hii ya
mboga husaidia kujaza tumbo na kufanya usihisi njaa haraka. Mfano wake ni viazi
(mviringo na vitamu).
VI. Nyinginezo
Sehemu
nyingine za mmea ambazo hutumika kama mboga ni pamoja na jicho la ua
(cauliflower), mbegu (kunde na maharage), shina (tangawizi), chipukizo/kimea
(majani ya kunde, soybean).
Umuhimu wa vyakula vya jamii ya mboga mboga mwilini
Watu
hushauriwa kula vyakula vya jamii ya mboga mboga kwa wingi. Sababu kubwa ni
kutokana na faida za kiafya ambazo huletwa kutoka kwenye mboga mboga ambazo
haziwezi kupatikana kutoka kwenye vyanzo vingine. Mboga zina vitamins na
madini (minerals) kama vile potassium, vitamin A & C
hupatikana kwa wingi kwenye mboga mboga na huhitajika mwilini kila siku ili
kuusaidia kuwa na afya na kuweza kukinga au kuzuia maradhi. Virutubisho vingine
husaidia kukinga moyo na figo dhidi ya maradhi na huzuia kansa.
Kanuni bora za ukuzaji wa mboga mboga
1. Kuchagua eneo
Katika
kuchagua eneo kwaajili ya kupanda mboga ni muhimu kuzingatia vitu vifuatafvyo;
·
Mwinuko: Eneo lisiwe kwenye mwinuko mkali kwa sababu husababisha mmomonyoko
wa udongo. Endapo sehemu itakuwa na mwinuko, tengeneza makingamaji ili kuzuia
mmomonyoko.
·
Udongo: Chagua udongo ambao una rotuba na wenye uwezo wa
kupitisha maji kwa urahisi.
·
Chanzo cha maji: Eneo la Bustani liwe karibu na maji ya kudumu au
chanzo cha maji ili kurahisisha umwagiliaji na maji yasiwe na chumvi nyingi
kwani huathiri ukuaji wa mimea.
·
Kitalu: Kisiwe mahali palipo na kivuli kingi kwani husababisha
mimea kutokupata mwangaza wa jua na kushindwa kutengeneza chakula hivyo kuwa
dhaifu.
·
Kuzuia upepo mkali: Upepo mkali huharibu mimea, kuvunja majani na
matawi na husafirisha vimelea vya ugonjwa na wadudu. Eneo la Bustani lioteshwe
miti mipakani ili kuzuia upepo mkali.
2. Kutayarisha shamba
Wakati
wa kulima ni muhimu kukatua udongo katika kina cha kutosha, mabonge yalainishwe
ili kurahisisha upitaji wa maji na hewa katika udongo. Wakati wa kiangazi,
tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya maji yaweze kukaa kwenye
udongo na wakati wa masika matuta yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi
ili kuzuia maji yasituame.
3. Kutumia mbegu bora
Mbegu
bora ni zile zilizokomaa na kukauka vizuri, ambazo hazijashambuliwa na magonjwa
au wadudu na zenye uwezo wa kuota vizuri zikipandwa. Inashauriwa kununua mbegu
kutoka kwa wakala halali.
4. Kuotesha na kupanda mboga
Kina
cha kuotesha mbegu kinategemea na ukubwa wa mbegu yenyewe. Mbegu ndogo,
hupandwa katika kina kifupi zaidi kuliko mbegu kubwa. Baadhi ya mbegu huoteshwa
kwanza kwenye kitalu kisha mche huhamishiwa bustanini au shambani.
5. Kumwagilia maji
Hakikisha
udongo una unyevu nyevu wa kutosha wakati wote na mmea unapata maji. Epuka
kumwagilia maji mengi sana kwani husababisha miche au mbegu kuoza.
6. Kuweka kivuli na matandazo
Utandazaji
wa majani makavu na uwekaji wa kivuli ni muhimu ili kuzuia jua linaloweza
kunyausha miche. Matandazo huhifadhi unyevu, joto la udongo na hupunguza palizi
ya mara kwa mara.
7. Matumizi ya mbolea
Mboga
hustawi vizuri zaidi katika udongo uliowekwa samadi, mboji au mbolea vunde ya
kutosha huwekwa kwenye udongo kabla ya kupanda au kupandikiza mimea. Debe moja
huhitajika kwenye tuta lenye upana wa mita moja. Mbolea huuongezea mmea
virutubisho na kuufanya ukue na kuzaa vizuri.
8. Kubadilisha mazao
Utaratibu
huu ni ule wa kuacha kupanda mfululizo aina ile ile ya zao katika eneo moja.
Inashauriwa kubadilisha aina ya zao ili kusaidia kupunguza kuenea kwa magonjwa
na wadudu na pia kuhifadhi rotuba ya udongo.
9. Matunzo mengineyo
Kupalilia
na kukatia mimea pale inapohitajika ni muhimu sana kwani magugu hufanya mimea
isikue vizuri kwa kutumia virutubisho kutoka kwenye udongo.
10. Kuvuna
Mboga
nyingi za majani hutakiwa kuvunwa kabla hazijakomaa sana. Baada ya kuvuna,
inashauriwa kuweka mboga kwenye eneo safi na salama ili kuweza kuzuia magonjwa
yatokanayo na vyakula. Kumbuka kuosha mboga kabla ya kula au kupika.
No comments:
Post a Comment